IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Njama za Marekani dhidi ya Quds hazifiki popote

12:59 - January 17, 2018
Habari ID: 3471357
TEHRAN (IQNA) Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Marekani imekuwa ikifanya "ufidhuli mkubwa" kuhusu Quds Tukufu (Jerusalem) na kuongeza kuwa njama zake hizo hazitafika popote.

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo alasiri mjini Tehran alipokutana na kufanya mazungumzo na wageni walioshiriki katika  kikao cha 13 cha maspika wa mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na kusema, 'kadhia ya Palestina ni kadhia yenye umuhimu wa kwanza katika ulimwengu wa Kiislamu." Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, katika kadhia ya Palestina, kuna matukio matatu yaliyojiri ambayo ni, 'kukaliwa kwa mabavu ardhi,' 'kubaidishwa kwa umati mamilioni ya watu' na 'kuuawa kwa umati pamoja na jinai kubwa dhidi ya binadamu'. Amesema matukio hayo hayana kifani katika historia.

Ayatullah Khamenei amesema kutetea Palestina ni jukumu la wote na kusisitiza kuwa: "Haipaswi kuwepo na taswira kuwa kukabiliana na utawala wa Kizayuni ni jambo lisilo na faida bali kwa idhini na uwezo wake Mwenyezi Mungu, jihadi ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni itakuwa na tija kama ambavyo harakati ya muqawama ilipiga hatua katika miaka ya nyuma."

Wasaudia wanawafanyia Waislamu uhaini

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: "serikali za eneo ambazo zinaisaidia Marekani na kushirikiana na utawala wa Kizayuni ili kuwakandamiza ndugu Waislamu zimetenda uhaini wa wazi na hilo ndilo jambo ambalo Wasaudia wanafanya."

Ayatullah Khamenei amesema Wazayuni wakati mmoja walikuwa wakitoa nara ya 'Kutoka Nile hadi Furat' lakini sasa wanalazimika kujenga ukuta kujilinda. Amesisitiza kuwa, hakuna shaka kuwa Palestina ni majumui ya historia ya 'Kutoka Bahari (ya Mediterania) hadi Mto (Jordan)' na Quds ni mji wake mkuu na hakuna uwezekano wowote  wa kufuta au kutia doa katika ukweli huo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kujadiliwa kadhia za Myanmar na Kashmir katika kikao cha maspika wa mabunge ya nchi za Kiislamu na kusema pia hakupaswi kusahauliwa kadhia muhimu za Yemen na Bahrain katika kikao hicho. Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, katika miaka ya nyuma, vyombo vikubwa na hatari vya habari vya nchi za Magharibi ambavyo kimsingi vinasimamiwa na Wazayuni, vimekuwa vikipuuza masuala muhimu ya Ulimwengu wa Kiislamu na kupitia njama ya kunyamaza kimya, vimekuwa vikifunika kadhia asili ya umma wa Kiislamu.Njama za Marekani dhidi ya Quds hazifiki popote

Ayatullah Khamanei amesisitiza kuhusu ulazima wa nchi za Kiislamu kuwa na mshikamano zaidi na kuongeza kuwa: "Hatupaswi kuruhusu hitilafu, vita na umwagaji damu katika ulimwengu wa Kiislamu, ambavyo wachochezi wakuu wake ni Wamarekani na Wazayuni, viwe chanzo cha kuuandalia mazingira salama utawala wa Kizayuni."

Matamshi ya Trump dhidi ya Waafrika, misdaki ya ukiukwaji haki za binadamu

 Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria madai ya Marekani ya kuunga mkono haki za binadamu na kusema: "Mtu ambaye anatawala Marekani anatangaza kwa uwazi kabisa misimamo ya nchi yake; tab'an hiyo imekuwa misimamo ya Marekani tokea nyuma lakini hawakuwa wakiitangaza wazi na mfano wa wazi wa kadhia hii ni matamshi yake ya hivi karibuni kuhusu Afrika na Amerika ya Lakini na watu wa rangi zingine." Kiongozi Muadhamu amesema matamshi hayo ya Trump ni misdaki ya ukiukaji wa haki za binadamu na kwa msingi huo hadaa ya Marekani inapaswa kufichuliwa.

Ayatullah Khamenei amesema madai mengine yasiyo na ukweli wowote ya Marekani ni kadhia ya vita dhidi ya ugaidi. Amesema  kuna ulazima wa kuweka wazi suala la uongo uliopo katika madai ya Marekani ili walimwengu na wasomi waweze kufahamu uhakika wa mambo.

Ustawi wa elimu

Kiongozi Muadhamu pia alisisitiza udharura wa nchi za Kiislamu kustawi katika uga wa elimu  na kusema Madola ya magharibi yameweza kupata utajiri na nguvu za kimataifa kupitia  elimu lakini kwa ajili hawana Imani wametumia vibaya uwezo huo kueneza dhulma na ubeberu. Aliongeza kuwa: "Ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuchukua hatua  za kuhakikisha vijana Waislamu wanastawi kielimu. Hapa Iran tumweza kuchukua hatua hiyo na hivi sasa nchi yetu imefanikiwa kustawi kielimu pamoja na kuwepo vikwazo ambavyo vimetulazimu kujitegemea. Leo Iran imepiga hatua katika nyuga kama vile za tiba, nano teknolojia ,seli shina, teknolojia  ya nyuklia n.k. Kati ya hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa katika nchi za Kiislamu ni kustawisha elimu na tusaidiane katika hili. Kwa bahati nzuri baadhi ya nchi za Kislamu tayari zimepiga hatua nzuri kielimu."

3464965

captcha