IQNA

Saudia yawazuia Waqatari kutekeleza Ibada ya Umrah

15:38 - January 07, 2018
Habari ID: 3471345
TEHRAN (IQNA)-Utawala wa Saudi Arabia unawazuia raia wa Qatar kutekeleza Ibada ya Umrah katika miji mitakatifu ya Makkah na Madinah.

Kwa mujibu wa taarifa, hivi karibuni raia 20 wa Qatar walikwama katika uwanja wa ndege wa Jeddah kwa siku mbili na baada ya kuzuiwa kuingia Saudia kutekeleza Ibada ya Umrah. Hatimaye baada ya kusumbuliwa sana walipelekwa Kuwait kwa sababu hakuna safari za moja kwa moja za ndege baina ya Qatar na Saudia.

Uamuzi huo wa Saudia umelaaniwa vikali katika mitandao ya kijamii huku wakosoaji wakisisitiza kuwa nchi hiyo haina haki ya kuwazuia Waislamu kutekeleza ibada katika miji ya Makka na Madina kwani miji hiyo ni milki ya Waislamu wote duniani.

Itakumbukwa kuwa Tarehe 5 Juni mwaka jana, Saudi Arabia iliongoza kundi la nchi nne za Kiarabu yaani Misri, Imarati na Bahrain pamoja na Saudia yenyewe, kuiwekea vikwazo vya kila namna Qatar ikiwa ni pamoja na kuifungia nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi mipaka yake yote ya nchi kavu, angani na baharini. Nchi hizo nne za Kiarabu zilidai kuwa, Qatar haikubali kufuata siasa za mrengo huo wa Kiarabu unaoongozwa na Saudi Arabia. Nchi hizo zinazoongozwa na Saudia zinataka Qatar ivunje uhusiano wake wa karibu na harakati za Ikhwanul Muslimin ya Misri na Hamas ya Palestina.

Aidha kati ya mambo mengine zinaitaka pia Qatar ipunguze au ikate kabisa uhusiano na Iran na ifunge televisheni yake ya Al Jazeera. Hatahivyo Qatar imekataa kutekeleza matakwa hayo na kusema ina mamlaka ya kijitawala na haiwezi kuruhusu wengine waiamulie mambo yake.

captcha